MAAFISA WATENDAJI KATA 21 KUWAPONGEZA VIONGOZI NGAZI YA WILAYA KWA TUZO MAALUMU, WANGING’OMBE.
Tarehe iliyowekwa: October 7th, 2025
Na. Nickson Kombe,
MAAFISA Watendaji wa Kata 21 za Halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe wamewapongeza viongozi ngazi ya wilaya kwa tuzo maalumu akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Katibu Tawala na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kwa namna ambavyo wanapata ushirikiano, usimamamizi na mafunzo zaidi kutoka kwa viongozi hao.
Akitolea ufafanuzi wa hafla hiyo, Mwenyekiti wa Watendaji wa Kata, Bw. Festo Mbakilwa ametoa historia na maendeleo ya Halmashauri tangu ilipoanzishwa rasmi 2013 ambapo watendaji baadhi walitokea Njombe na baadae uwepo wa viongozi Hodari walioweza kuleta mapinduzi na kuifikisha Halmashauri ya Wanging’ombe hapo ilipo.
Hata hivyo ametoa pongezi na shukrani za dhati dhidi ya safu ya viongozi ngazi ya wilaya akinukuliwa kusema “……. Tangu amekuwa mtumishi wa umma hajawahi kupata ushirikiano, uongozi na uratibu mzuri zaidi kama viongozi waliopo sasa 2025, kwake imekuwa ni neema kukutana na Mkuu wa wilaya, Katibu Tawala na Mkurugenzi Mtendaji ambao wanahakikisha kila mtumishi anapata haki zake na wananchi wanapata huduma bora na maendeleo” ameyasema hayo Mwenyekiti wa Watendaji Kata, Bw. Mbakilwa.
Kwa upande wa Viongozi wamepewa fursa ya kutoa neno katika hafla hiyo iliyosindikizwa na visinia vya kibabe katika Ukumbi wa Mianzi Kempu, Igwachanya, ambapo Mkuu wa Wilaya amesema kitendo cha kupokea tuzo hizo maalumu, kwao zitabaki kuwa kumbukumbu nzuri ambazo zimeonyesha katika vipindi vyao vya uongozi wamegusa maisha wa watu anaowaongoza na kuacha alama, hivyo ameshukuru kupata tuzo hizo.
Aidha Mtendaji Kata, Bi. Agatha akiwakilisha watendaji wenzake amesema hivi sasa upatikanaji wa haki za watumishi umeboreka zaidi na kwake yeye ameshuhudia kupata kipaumbele aendapo ofisi za Mkurugenzi Mtendaji kitu ambacho kinampa faraja na Fahari ya kupata huduma bora kutoka kwa kiongozi huyo, pia ameahidi kukusanya mapato ili kufikia malengo kadiri iwezekanavyo.