Naibu Waziri Mkuu pia Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko ametembelea na kukagua baadhi ya Miradi ya Umeme Vijijini "Kijiji cha Ikwavila" Kijombe inayosimamiwa na REA pamoja na Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Njombe "Njombe Girl's" iliyopo Kijiji cha Usalule kata ya Ulembwe.
Akihotubia Wananchi wa Kijiji cha Ikwavila, Kijombe, Mhe. Dkt. Dotto Biteko amesema Wilaya ya Wanging’ombe yenye vijiji 108 vyote vimekwishafikiwa na miundombinu ya umeme kupitia mradi unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini REA (R3R2) ambapo zimetumika zaidi ya Fedha za Kitanzania Bilioni 9.5 kwa ajili ya kusambaza umeme Vijiji vya Wilaya ya Wanging'ombe.
Pia Mheshimiwa Dkt. Biteko ametembelea kiwanda cha kuchakata nguzo TANWAT, Ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuifungua Wilaya ya Wanging’ombe katika Nyanja zote.
Naibu Waziri TAMISEMI pia Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe, Mhe. Dkt. Festo Dugange amemshukuru Mhe. Dkt. Biteko 'Naibu Waziri Mkuu' kutembelea na kukagua shughuli mbalimbali za kimaendeleo Wilaya ya Wanging’ombe, ambapo ameahidi kuwezesha laini ya umeme kubwa zinazojitegemea, kuongeza vifaa ambavyo vitasaidia kuepusha hitilafu na kutenga laini ili kuzuia eneo kubwa kuathirika kwa hitilafu hizo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa REA, Bw. Geofrey Chibulunje amesema Miradi ya Umeme Vijijini inayosimamiwa (REA), ipo Miradi mitatu, REA Tatu Mzunguko wa Pili (R3R2) Ujazilizi (2B) yenye lengo la kufikia miundombinu ya umeme kwenye Huduma mbalimbali za kijamii kama vile Vituo vya Afya na Pampu za Maji (RUWASA na WANGIWASA).
Aidha Mhe. Dkt. Biteko amefurahishwa kukutana na wazalishaji wadogo wenye kuonesha tija ya uzalishaji umeme na kutoa ahadi ya kuwawezesha kununua umeme huo huku akiwatoa wasi Wananchi kuhusu Mpango mkuu wa Taifa wa Uzalishaji umeme kwa kutumia maji, ambapo muda wowote kuanzia sasa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP) litaunganishwa na Gridi ya Taifa na kupunguza makali ya mgao wa umeme.