MCHUNGAJI AJITOLEA UKAMILISHAJI WA MADARASA MAWILI, S/M LUGODA
Tarehe iliyowekwa: October 7th, 2025
Na. Nickson Kombe,
MCHUNGAJI Daktari Benson Gudaga amejitolea kuchangia kiasi cha milioni 25 kukamilisha ujenzi wa madarasa mawili ya Shule ya msingi Lugoda kata ya Usuka wilayani Wanging’ombe.
Akitolea ufafanuzi huo, Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe, Mhe. Zakaria Mwansasu wakati wa makabidhiano na uzinduzi wa mradi huo, amepongeza hatua hizo zilizofanywa na Mchungaji Daktari Gudaga akishirikiana na wadau mbalimbali pamoja na wananchi wa eneo hilo.
“……. Katika kumbukumbu zangu sijawahi kuona/kusikia Mchungaji amejitolea na kurejesha kwenye jamii kupitia ujenzi wa madarasa haswa Shule za msingi, Hongera sana Daktari Gudaga, wadau na wananchi wote wa eneo hili, sasa nakabidhi madarasa haya kwenye uongozi wa shule ili yaanze kutumika rasmi” alisema Mkuu wa wilaya ya Wanging’ombe.
Ikumbukwe madarasa hayo yameanza kujengwa kwa mchango na nguvu kazi ya wananchi wa Kijiji cha Lugoda ikiwa yanasimamiwa na Mhandisi wa Halmashauri, ambapo hatua za umaliziaji wa majengo hayo umefanyika na Mchungaji Daktari Gudaga kupitia mchango wake wa pesa taslimu 25,110,000.
Aidha Mwenyekiti wa Kijiji cha Lugoda akiwakilisha wananchi wa Kijiji hiko ametoa neno la shukrani kwa Mchungaji Gudaga na kuomba aendelee na jitihada za kuwezesha miradi mbalimbali kijijini hapo Kadiri atakavyoweza.