DC AAHIDI MATENGENEZO YA BARABARA ZA IVIGO – WANGING’OMBE
Tarehe iliyowekwa: October 2nd, 2025
Na. Nickson Kombe,
MKUU wa wilaya ya Wanging’ombe, Mhe. Zakaria Mwansasu aahidi matengenezo ya Barabara mbili tofauti zenye jumla ya kilomita 17.47 kiwango cha changarawe za Kijiji cha Ivigo kata ya Igosi wilayani wanging’ombe.
Akiongea na wananchi wa Kijiji cha Ivigo, Jumanne 30 Septemba 2025, katika mkutano wa kikazi wa kutembelea vijiji 108 wilayani humo, Mhe. Mwansasu ametoa fursa ya kusikiliza changamoto za wananchi kijijini hapo na moja ya changamoto hizo ni ubovu wa Barabara za Idunda-Ivigo-Igosi (Kilomita 9.4) na Barabara ya Ivigo-Igodivaha (Kilomita 8.07). Barabara hizo ni msingi wa maendeleo ya kijiji cha Ivigo kwa sababu hutumika kusafirishia mazao ya mbalimbali kama parachichi, viazi, ngano na mahindi.
Mhe. Mwansasu aahidi matengenezo ya Barabara hizo ili kuendeleza ustawi na maendeleo ya kijiji hiko na kuwataka wananchi hao kuendelea kufanya shughuli za maendeleo kama kilimo ambapo Serikali itaendelea kushughulikia changamoto ya pembejeo za kilimo haswa bei za mbolea za mazao.
Akitolea ufafanuzi wa hatua za matengenezo ya Barabara hizo, Kaimu Meneja wilaya ya Wanging’ombe-TARURA, Mhandisi Anesporo Mwijuka amesema tayari Serikali imetenga kiasi cha milioni 138 kutengeneza Barabara ya Idunda-Ivigo-Igosi yenye kilomita 9.4 na kiasi cha milioni 134.2 kimetengwa kutengeneza Barabara ya Ivigo-Igodivaha yenye kilomita 8.07. Hatua iliyopo kwa sasa tayari Mkandarasi amepatikana taratibu za matengenezo zitaendelea muda mfupi ujao.
Aidha wananchi wa Kijiji cha ivigo wakiwakilishwa na Mwenyekiti wa Kijiji wamesema ubovu wa Barabara hizo unapelekea uuzwaji wa mazao kwa bei ndogo ukilinganisha na maeneo mengine hivyo wamesisitiza ukamilishaji wa matengenezo ya Barabara hizo kwa haraka zaidi ili kuondokana na bei ndogo za mazao yao.