ZIARA YA KAMATI YA MAENDELEO, UONGOZI NA MIPANGO (KFUM) KURIDHISHWA NA UTEKELEZAJI MRADI WA UJENZI WA MADARASA KIDATO CHA 5 NA 6, SHULE YA SEKONDARI, MOUNT KIPENGERE
Tarehe iliyowekwa: October 16th, 2023
Na. Nickson Kombe,
16 Oktoba 2023.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo, Uongozi na Mipango, Mhe. Onesmo Lyandala akiongozana na baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo ametoa pongezi kwa Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe katika usimamizi wa fedha mradi wa Ujenzi madarasa Shule ya Sekondari, Mount Kipengere.
Akitoa mrejesho baada ya kusomewa taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Mhe. Onesmo Lyandala amesema wataalamu waendelee kutoa msaada wa ushauri ili kupunguza dosari za ujenzi zisizokuwa na ulazima pindi mradi huo unapoenda kukamilishwa.
Mkurugenzi Mtendaji, Wilaya ya Wanging'ombe, Bi. Maryam Muhaji akitolea ufafanuzi ujenzi wa mradi huu wenye thamani jumla ya Shilingi Milioni 742 ambapo utahusisha ujenzi wa vyumba vya madarasa - 8, matundu ya vyoo - 11, mabweni ya wavulana - 2, mabweni ya wasichana - 2 (SEQUIP) unatarajiwa kukamilika Disemba 2023.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati hiyo wametoa ushauri wa namna bora ya usimamizi wa mradi huo ili kupunguza dosari ndogondogo za ujenzi zinazojitokeza katika hatua za umaliziaji wa ujenzi.
Aidha Kamati hiyo imeridhishwa na maendeleo ya mradi huo wa ujenzi na kusisitiza mchango na ushirikiano wa watalaamu kujitolea zaidi ili kufanikisha kukamilika kwa mradi huo.
Mkuu wa Shule, Mwl. Belnow Mhanga ametoa pongezi na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za dhati kuboresha sekta ya elimu, pamoja na Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Mbunge wa Jimbo la Wanging'ombe, Mhe. Dkt Festo Dugange na Diwani wa Kata ya Kipengere, Mhe. Mussa Sanga kwa ufuatiliaji wa karibu kipindi cha utekelezaji wa mradi.