WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua mradi wa maji katika kijiji cha Bwasa katika mji wa Nansio wilayani Ukerewe na kuuagiza uongozi wa wilaya hiyo kuhakikisha maji hayo yanatoka wakati wote na mradi huo unakuwa endelevu. Waziri Mkuu alizindua mradi huo jana (Jumapili, Februari 18, 2018) wakati akiwa katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza. Alisema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama nchini.
Baada ya kuzindua mradi huo, Waziri Mkuu alizungumza na wananchi wa mji wa Nansio kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Getrude Mongella, ambapo alisema mradi aliouzindua katika kijiji cha Bwasa ni sehemu ya mradi wa maji wa Kazilankanda utakaohudumia vijiji 13 vya wilaya hiyo.
Alisema mradi huo unagharimu shilingi bilioni saba na unatekelezwa katika vijiji vya Muhula, Mahande, Namasabo, Namagondo, Kazilankanda, Malegea, Igalla, Kigara, Lutare, Busunda, Bwasa, Buhima, Hamuyebe na utahudumia wakazi 68,038 pindi utakapokamilika.
Mkataba wa Mradi huo ulisainiwa Machi 2013 na unatarajiwa kukamilika ifikapo April, 2018, ambapo hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 5.637 sawa na asilimia 78.26 tayari zimeshatumika na mradi umekamilika kwa asilimia 92 na tayari baadhi vijiji vimeanza kupata maji.
Waziri Mkuu alisema mkakati wa Serikali ni kuwahudumia wananchi kwa kutatua kero zinazowakabili ikiwemo ya upatikanaji wa maji, ambapo imedhamiria kuendelea kusambaza huduma hiyo hadi vijijini ili kuhakikisha vyote vinapata maji.
Waziri Mkuu alisema Serikali inatekeleza Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Waziri Mkuu aliwaambia wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kuondoa tatizo la maji kote nchini ili kusaidia wananchi hao hasa wanawake kutumia muda mwingi kufanya kazi za maendeleo kuliko kutafuta maji.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Bw. Estomihn Chang’ah apange siku maalumu kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi hususani za ardhi na kushirikiana nao katika kuzipatia ufumbuzi.
Pia Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu huyo wa wilaya leo saa 3.00 asubuhi akiwa na watumishi wa Idara ya Ardhi akutane na wananchi wote wenye malalamiko ya ardhi ili ashirikiane nao katika kuyapatia ufumbuzi. Alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko mengi ya wananchi yahusuyo masuala ya ardhi yaliyowasilishwa kwake kupitia njia ya mabango.
Alisema kwa sababu ya kutotekeleza wajibu wao ipasavyo kumekuwa na kero na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi na hivyo kusababisha wananchi kuwasilisha kero na malalamiko hayo wakati wa ziara za viongozi wakuu wa nchi.
Awali, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bw. Luhaga Mpina aliwaomba wananchi hao kutunza rasilimali zilizopo ndani ya ziwa Victoria na kujiepusha na uvuvi haramu kwa sababu unatishia uwepo wa samaki ndani ya ziwa hilo.
Waziri huyo alisema iwapo vitendo vya uvuvi haramu vikiachwa bila ya kuzuiwa kuna uwezekano mkubwa wa samaki kutoweka ndani ya ziwa hilo baada ya miaka miwili. Alisema tayari Serikali inaendelea na operesheni ya kupambana na uvuvi haramu.
(mwisho)IMETOLEWA NA:OFISI YA WAZIRI MKUU,JUMATATU, FEBRUARI 19, 2018.
Copyright ©2021 Wanging'ombedc . All rights reserved.