WATUMISHI WA IDARA YA AFYA WAKUMBUSHWA MAADILI YA KAZI – WANGING’OMBE
Tarehe iliyowekwa: November 9th, 2023
Na Mwandishi Wetu,
Rukia Omary,
Mkurugenzi Mtendaji, Wilaya ya Wanging’ombe, Bi. Maryam Muhaji amewaasa Watumishi wa Idara ya Afya kuendelea kuzingatia sheria na maadili ya kazi ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi katika vituo vyao vya kazi wilayani Wanging’ombe.
Akitolea ufafanuzi baada ya kualikwa kwenye kikao kazi, Mkurugenzi Mtendaji, Wilaya ya Wanging’ombe, Bi. Maryam Muhaji amesema ni wajibu wa Mtumishi wa umma kuzingatia Sheria za Utumishi wa umma. “Sekta ya Afya ni msingi wa afya bora kwa watu hivyo ni sekta nyeti na inahitajika watumishi wenye weledi na kuzingatia maadili yao ya kazi ili kutoa huduma bora kwa wananchi”. Ikiwa baadhi ya Watumishi wa Afya wanakiuka kanuni na maadili yao ya kazi ni hatari katika Ustawi wa jamii yetu. Hivyo watachukuliwa hatua kali za kinidhamu ili kuhakikisha wanabadilika na kufanya kazi kwa kuzingatia weledi.
Kwa upande wa Afisa Rasilimali Watu, Wilaya ya Wanging’ombe, Bi. Odetha Baninge amesema Mtumishi anapaswa kuzingatia aina ya mavazi yenye kuendana na eneo lake la kazi, uadilifu kazini. Tabia za wizi wa dawa na vitendea kazi ni marufuku, kutokuheshimu mamlaka zilizopo, rushwa kuvujisha siri za wagonjwa.
Akiendelea kwa kutilia mkazo, Mganga Mkuu, Wilaya ya Wanging’ombe, Dkt. Frank Chiduo amesema maadili na weledi kazini ni jambo linalosimamiwa na waganga wafawidhi hivyo haina budi kuheshimu mamlaka hayo waliyopewa katika vituo vyao vya kazi ili kujenga mahusiano mazuri baina ya watumishi na jamii iliyopo karibu na vituo vya afya.
Aidha watumishi wa Idara ya Afya, Wilaya ya Wanging’ombe wametoa neno la Shukrani baada ya kukumbushwa maadili ya kazi. Katibu Afya Hospitali ya Wilaya, Zuhura Kalindima akiwawakilisha watumishi wengineo amesema watazingatia maelekezo waliyopewa na viongozi.