Timu ya Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe, imeshiriki bonanza, ili kujiweka tayari kwa ajili ya Mashindano ya Timu za Watumishi wa Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA), yanayotarajia kuanza kutimua vumbi Agosti 15, 2025 jijini Tanga.
Akiongea mara baada ya kuwasili katika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Wasichana mkoa wa Njombe Julai 26, 2025, Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni, Michezo na Sanaa, Bi. Anitha Kivike ambaye pia ni msimamizi wa timu ya Watumishi Halmashauri ya wilaya ywa Wanging’ombe amesema, wameamua kujiandaa kwa utaratibu rafiki kuendana na mazingira ya Bonanza hilo maalumu ikiwa ni fursa ya kujiimarisha kwa ajili ya Mashindano yajayo ya SHIMISEMITA.
Kadhalika, katika Bonanza hilo zimechezwa mechi kadha wa kadha baina ya timu rasmi ya watumishi ikijiimarisha dhidi ya timu za wanafunzi wa Sekondari pamoja na timu za vijiji vya Usalule kata ya Ulembwe ambapo matoke oni kama ifuatavyo; Kuvuta Kamba, ambapo timu ya Wasichana ya Sekondari imeshinda dhidi ya Watumishi, kwa upande wa Wanaume, timu ya Watumishi wameshinda dhidi ya Wanakijiji, mchezo wa mpira wa miguu, Watumishi wameshinda 1 – 0 dhidi ya Usalule Heros, Handball; Timu ya Wasichana Njombe Girl’s imeongoza 6 – 4 dhidi ya Watumishi na Volleyball; Usalule Volleys imeshinda Set 2 kati ya 3 dhidi ya Watumishi.
Aidha, Bi. Anitha Kivike amesema ya kuwa Mashindano ya SHIMISEMITA mwaka huu yanatarajiwa kuwa na ushindani na msisimko wa kipekee kwani ushiriki wa timu mbalimbali za Watumishi umekuwa ukiongezeka kwa kila awamu kutokana na Hamasa inayoenda sambamba na tukio adhimu la Uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, pamoja na dhamira ya kuwakutanisha Watumishi ili kupeana maarifa na uzoefu na kuimarisha afya ili kuimarisha weledi katika majukumu yao, mashindano ya Mwaka huu yataenda kwa kauli mbiu madhubuti ya kuelimisha na kuwakumbusha Watanzania haki yao ya Kikatiba ya kuchagua Viongozi wao isemayo "Jitokeze Kupiga Kura kwa Maendeleo ya Michezo".