WANANCHI UJINDILE WATAKIWA KUCHANGIA GHARAMA NDOGO ZA MAJI.
Tarehe iliyowekwa: October 2nd, 2025
Na. Nickson Kombe,
WANANCHI Kijiji cha Ujindile kata ya Igosi wilayani Wanging’ombe watakiwa kuendelea kuchangia gharama ndogo za maji ikiwa lengo ni kuhakikisha mradi huo wa huduma ya maji unaendelea kuwahudumia katika ubora zaidi.
Akiongea na Wananchi hao, Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Mhe. Zakaria Mwansasu ametumia fursa hiyo kutoa elimu na kuhamasisha wananchi hao kuendelea kuchangia Chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs) ili itakapo tokea matengenezo au gharama za uendeshaji wa mradi huo wa maji basi michango yao itasaidia kurejesha huduma ya maji katika ubora zaidi.
Mhe. Mwansasu ameyasema hayo alipokuwa ziara ya kikazi kutembelea vijiji 108, ambapo tarehe 30 septemba 2025 ametembelea kata ya Igosi katika vijiji vya Ujindile na Ivigo ikiwa lengo ni kuendelea kusikiliza kero na kuzitafutia ufumbuzi pamoja na kuongea na wananchi kuhusu shughuli mbalimbali za maendeleo yao.
“………. ninawasihi kuendelea kuchangia gharama ndogo za maji ambazo mnapangiana kulingana na mazingira yenu…….” Amesisitiza Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Mhe. Mwansasu.
Kwa sasa Hali ya upatikanaji wa Maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe imefikia zaidi asilimia 88 ambapo zaidi ya kaya 5500 wanapata huduma hiyo huku mkakati unaotazamiwa baada ya ukamilishaji wa mradi wa maji wa miji 28 utaenda kuwafikiwa watumiaji wengi zaidi.