MKUU wa Wilaya ya Wanging’ombe, Mhe. Zakaria Mwansasu amewataka wananchi hususani wanaojishughulisha na kilimo kuepuka kuchoma moto mashamba na badala yake watumie mbinu mbadala kuandaa mashamba na kuendelea kuhifadhi mazingira.
Ameyasema hayo wakati akiwa ziara ya kikazi kata za Mdandu, Luduga, Malangali, Uhenga na Saja, hata hivyo hivi karibuni zaidi ya Ekari 360 sawa na thamani ya shilingi milioni 340 yenye miti, nguzo 8 za laini kubwa yenye msongo wa kilovolti 33 na mazao mengineyo imeathiriwa na uchomaji moto holela wakati wa usafishaji mashamba katika kata za Kipengele, Ulembwe, Makoga na Wangama.
Akiendelea kutolea ufafanuzi namna bora ya kuandaa mashamba, Mhe. Mwansasu amesema haoni sababu za msingi za mkulima kuchoma moto mabua hali ambayo inahatarisha ustawi na rotuba ya ardhi, mali za watu zinazozunguka maeneo hayo. Akitolea mfano wa tofali zilizochomwa moto iwapo udongo wake ukitumika kupanda mahindi, yatastawi…?? Hata hivyo ametoa njia sahihi ya maandalizi ya shamba kwa kufukia mabua, magugu na vichaka ambapo huoza na kuzalisha mbolea ya mboji ambayo itapelekea ustawi mzuri wa shamba na matumizi ya mbolea kwa kiasi ili kukuzia mazao.
Aidha Wananchi wanapaswa kujihadhari na uchomaji moto holela katika maeneo ya mashamba sambamba na kuondoa imani potofu za kuchoma moto kunaongeza rotuba ilihali zoezi hilo hutokomeza bakteria waliopo ardhini na kufubaza udongo.