DC MWANSASU: NUNUENI MBEGU ZA MAHINDI KUTOKA MADUKA RASMI – WANGING’OMBE
Tarehe iliyowekwa: November 15th, 2024
Na. Nickson Kombe,
MKUU wa Wilaya ya Wanging’ombe, Mhe. Zakaria Mwansasu amewataka wakulima wote wa mahindi kufanya manunuzi ya mbegu za mahindi kutoka maduka rasmi yenye vibali vya uuzaji wa pembejeo na kutunza risiti zao ili kuepukana na hasara zinazoweza kujitokeza iwapo ustawi wake hautoendana na viwango vinavyohitajika.
Mhe. Mwansasu ameyasema hayo alipokua akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa kata za Luduga na Malangali na kuwataka wakulima kuichangamkia fursa hiyo vizuri kwa kununua mbegu bora za mahindi kwa bei nafuu kutoka kwa wauzaji ili kuongeza uzalishaji wenye tija.
Amesema Muongozo wa Serikali kuanzia Septemba 24, 2024 umeweka bayana bei elekezi katika makundi matatu ya mbegu ambapo kuna Mbegu zinazochavushwa huria (Open Pollinated Varieties – OPV) Kilo 2 – 7,000/=, Mbegu Chotora au Hybrid (Zinazokomaa mapema/muda mfupi) Kilo 2 – 14,000/= na kundi la tatu ni Mbegu za Chotora (Zinazokomaa muda mrefu) Kilo 2 – 14,500/= aina kama DK 777, DKC 9086, PANNAR 691, SC 719 TEMBO na ZAMSEED 638.
Hata hivyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa ruzuku ya Mbegu bora za Mahindi kwa Wakulima ikiwa na lengo kuleta mageuzi na tija kwenye Sekta ya Kilimo, ili kuweza kumnufaisha mkulima kwa kupata uhakika wa chakula katika ngazi ya kaya na Taifa kwa ujumla.
Aidha Mbolea za Ruzuku zimeanza kutolewa kuanzia Julai 2024 na wakulima wilayani Wanging’ombe wanajulishwa ya kuwa Zoezi la Uhuishaji wa taarifa za Wakulima na Usajili wa wakulima wapya ili kupata Mbolea za ruzuku linaendelea.