VIJIJI 10 VYA WANGING'OMBE KUNUFAIKA NA HATI ZA KIMILA 3,010
Tarehe iliyowekwa: May 13th, 2025
Na. Nickson Kombe,
VIJIJI 10 vya wilaya ya Wanging'ombe kunufaika na hati za kimila 3,010, mradi ambao unatekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikishirikiana na Taasisi Lisilo lakiserikali la "Tanzania Land Tenure Assistance" – TLTA ikiwa lengo ni kutekeleza mkakati wa dira ya taifa wa kurasimisha ardhi yote ifikapo 2050.
Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Mlevela na Nyumbanitu, wakati wa hafla za makabidhiano ya hati hizo, Mkuu wa wilaya ya Wanging'ombe, Mhe. Zakaria Saili Mwansasu amesema anatarajia migogoro ya ardhi kupungua kwa kiasi kikubwa hivyo ulinzi na usalama wa wananchi utakuwa vizuri zaidi.
Katika siku ya hafla ya makabidhiano ya hati hizo tarehe 13 Mei, Mkuu wa wilaya ya Wanging'ombe, Mhe. Zakaria Saili Mwansasu amekabidhi jumla ya hati za kimila – 882 ambapo Kijiji cha Mlevela – 549 na Nyumbanitu - 333 akitumia fursa hiyo kuwaelimisha wananchi kuendelea kuboresha kufanya shughuli zao za kimaendeleo, watumie fursa za mikopo ya riba nafuu zilizopo kwenye taasisi za kifedha nchini.
Akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuisimamia na kutekeleza mipango ya urasimishaji wa ardhi yote ya Tanzania. Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe ametumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Mkurugenzi wa Taasisi Lisilo lakiserikali la "Tanzania Land Tenure Assistance" – TLTA, Bw. Mustapha Issa kwa uratibu wa zoezi lote la mradi wa urasimishaji ardhi ya wananchi wa wilaya ya Wanging’ombe.
Pamoja na Hayo, Wanufaika ya hati za kimila wa vijiji vya Mlevela na Nyumbanitu kata ya Igima wametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wataalamu wote waliohusika na mchakato huo.
Aidha Vijiji vinavyonufaika na mradi huu ni Mdasi, Kanani, Itowo, Samaria, Itambo, Ng’anda, Ihanzutwa, Utewele, Nyumbanitu na Mlevela kwa kukabidhiwa jumla ya hati za kimila 3,010.