UTAMBULISHO WA MRADI WA HUDUMA ENDELEVU ZA MAJI NA USAFI WA MAZINGIRA VIJIJINI - (SRWSSP)
Tarehe iliyowekwa: October 19th, 2023
Na. Rukia Omary,
Mkurugenzi Mtendaji, Wilaya ya Wanging’ombe, Bi. Maryam Muhaji akiambatana na wataalamu wa Idara ya Afya wamefanya utambulisho wa Mradi endelevu wa maji na usafi wa mazingira (SRWSSP) kwa viongozi, watendaji na watumishi kutoka vijiji lengwa katika Ukumbi wa Halmashauri.
Akitolea ufafanuzi wa utekelezwaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji, Wilaya ya Wanging’ombe, Bi. Maryam Muhaji amesema programu hii imeanzishwa ikiwa na dhumuni la kuboresha afya na mazingira ambapo itahusisha utoaji elimu ya Afya na usafi wa mazingira ngazi ya jamii, ujenzi wa miundombinu kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya katika zahanati ya Ulembwe, Ivigo, na Samaria. Shule za msingi Mhaji na Ulembwe utafanyika ujenzi wa miundombinu bora ya vyoo, matenki ya maji na kujenga vichomea taka.
Mganga Mkuu, Wilaya ya Wanging’ombe, Daktari Frank Chiduo ametolea ufafanuzi Mradi wa (SRWSSP) ikiwa na maana ya “Suistainable Rural Water Supply and Sanitation Program” unaogharimu jumla ya Shilingi Milioni 255.1 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu bora ya vyoo, matenki ya maji na kujenga vichomea taka katika vituo vya afya (Zahanati – 3) na Shule za Msingi 2.
Hata hivyo Afisa Afya Wilaya ya Wanging’ombe, Bw. Abdul Mwasumbi amesema kuwa ili kunufaika zaidi na mradi huu wa mbegu, Halmashauri imejipanga pindi mradi huu utakapokamilika kwa kupata zaidi ya shilingi milioni 399 ambazo zitaendeleza utekelezaji wa miradi mingine katika maeneo mengine.
Baadhi ya viongozi wa vijiji vinavyonufaika na mradi, maafisa watendaji wa kata na vijiji na watumishi wa umma kama wakuu wa shule wanaonufaika na mradi huu walitoa neno la Shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za dhati kuboresha afya na mazingira ya wananchi akishirikiana na Mbunge wa Jimbo la Wanging’ombe, Mhe. Dkt. Festo Dugange na madiwani kata za Ulembwe, Igima, Igosi na Makoga.