MKUU wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka ameagiza mkataba uliokuwa baina ya Kampuni ya udalali ya Ihagala Auction Mart na Halmashauri ya Mji wa Njombe wakufanya kazi ya kukusanya kodi na ushuru kutoka kwa wafanyabiashara uvunjwe.
Ole Sendeka ametoa agizo hilo juzi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe,Bi, Iluminata Mwenda baada ya kukutana na wafanyabiashara kwenye kikao kilichofanyika katika ukumbi wa turbo mjini Njombe.
"Sijaridhika na jinsi ambavyo kampuni ya Ihagala kwanza ilivyopatikana, imepatikana kwa kweli kwa mlango wa nyuma, haikufuata sheria ya manunuzi, lakini najua kuna mambo mazuri umeyafanya ya kusaidia ukusanyaji wa kodi, ukweli kampuni yenyewe na utendaji wa kazi, umegeuka kuwa kero kwa wafanyabiashara," alisema Ole Sendeka.
Alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Njombe kuzingatia sheria ya manunuzi katika kumpata mtu atakayesaidia ukusanyaji wa ushuru kwa wafanyabiashara.
"Mkataba uvunjwe haraka inavyowezekana, baada ya tarehe 28 Februari anza mchakato kaa na madiwani wako na wataalam wako, shaurianeni muone uwezekeno wa kukusanya kodi nyie wenyewe na ikishindikana mtangaze tenda ya wazi, ili madalali wote waweze kushindania na atakayeshinda akubali kufanya kazi kwa utaratibu ambao hata geuka kuwa tatizo kwa Njombe Mji," alisema Ole Sendeka.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Njombe, Onesmo Mwajombe alisema kilio kingi cha wafanyabiashara mkoani hapa kilikuwa ni kuilalamikia kampuni hiyo ya Ihagala kufanya kazi kwa kuwanyanyasa na kuwapiga wafanyabiashara wakati wanapokwenda kudai kodi na ushuru.
Naye Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya Ihagala auctin malt Caly Msango alisema kuwa tuhuma hizo si za kweli ila amekuwa akiisaidia halmashauri kukusanya mapato.
Miongoni mwa tuhuma ambazo kampuni hiyo imelalamikiwa ni ya wafanyakazi wanaokusanya ushuru na kodi kudaiwa kuchukua kiasi cha shilingi elfu hamsini kwa manufaa ya kampuni yenyewe.
"Kuna mtu unamkuta hana hela, Siyo elfu hamsini yote inachukuliwa, namwambia funga duka lako nenda kalipe leseni, kama ni ushuru analipa palepale," alisema Msango.
Copyright ©2021 Wanging'ombedc . All rights reserved.