MKURUGENZI MTENDAJI WANGING’OMBE, DKT. NYANJA APEWA TUZO YA UONGOZI BORA.
Tarehe iliyowekwa: September 3rd, 2025
Na. Nickson Kombe,
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe, Dkt. Peter Maiga Nyanja ametunukiwa tuzo maalumu na zawadi kwa kutambua mchango wake katika usimamizi wa taasisi, ambapo ameimarisha uwazi, uadilifu na uwajibikaji wakati wa kikao kazi na watendaji 108 wa vijiji vya wilaya ya Wanging’ombe kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri.
Mwenyekiti wa Umoja wa Watendaji wa Vijiji, Bi. Mariam Mbuji amemkabidhi Mkurugenzi Dkt. Nyanja tuzo hiyo leo Septemba 02, 2025, kwa niaba ya watendaji 108 wa vijiji ikiwa lengo ni kutoa neno la shukrani baada ya kuiongoza taasisi na kufikia lengo na kuzidi la ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha 2024/25 kutoka Bilioni 4 hadi Bilioni 6.
Hata hivyo Mkurugenzi Dkt. Nyanja amehamasisha watendaji hao kuendelea kukusanya mapato kadiri iwezekanavyo ili kufikia lengo na itabaki kwake utekelezeaji wa ununuzi wa pikipiki 108 za watendaji wa vijiji ili kurahisisha majukumu yao katika maeneo ya kazi.
Aidha Mwenyekiti wa Umoja wa Watendaji wa Vijiji, Bi. Mariam amesema nanukuu “Mnyonge mnyongeni ila haki yake mpeni….” kwa jinsi ambavyo Mkurugenzi Dkt. Nyanja ameongeza hamasa ya ukusanyaji mapato na kuwawezesha watendaji wa vijiji kufikia malengo kwa kuwapa mafunzo na mbinu mbalimbali za kukusanya mapato.