MKURUGENZI MTENDAJI, WANGING'OMBE AWEZESHWA KUSAFIRISHA WANAFUNZI WASIOONA KUSHIRIKI MAADHIMISHO YA FIMBO NYEUPE, NJOMBE MJINI
Tarehe iliyowekwa: October 20th, 2023
Na. Nickson Kombe,
Kuelekea kilele cha maadhimisho Siku ya Fimbo nyeupe ulimwenguni, Mkurugenzi Mtendaji, Wilaya ya Wanging’ombe, Bi. Maryam Muhaji awezeshwa kusafirisha wanafunzi wasioona na waalimu wao kushiriki Maadhimisho hayo siku ya Ijumaa, 24 Novemba 2023, Njombe Mjini.
Akitolea ufafanuzi kuhusu maadhimisho hayo, Bi. Maryam Muhaji, Mkurugenzi Mtendaji, Wanging’ombe amesema ni siku maalumu ambayo huadhimishwa kote ulimwenguni kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa macho (hasa wale waliopoteza uoni, yaani wasioona). Fimbo nyeupe, ni fimbo maalumu inayotumika na mtu asiyeona, ili kumtambulisha kwa watumiaji wengine wa barabara, wakati wowote na hasa anapokuwa akitembea.
Lengo la maadhimisho hayo, ni kuihamasisha jamii na watumiaji wote wa barabara kama vile madereva, kuiheshimu fimbo nyeupe na kumsaidia asiyeona anapotembea na anapovuka barabara. Pia siku hii hutumika kutambulisha shughuli mbalimbali zinazofanywa na wasioona, malengo yao, mahitaji yao, uwezo wao katika suala zima la maendeleo, changamoto wanazokabiliana nazo, na mchango unaohitajika toka Serikalini na wadau wengine wa maendeleo.
Afisa Elimu ya Msingi, Wanging’ombe, Bw. Gerald Kifyasi akiambatana na Afisa Elimu Maalumu, Wanging’ombe, Bw. Omega Kagine watoa neno la pongezi na shukrani kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Longolela Investment, Bw. John Longolela kwa kujitolea kuwasafirisha wanafunzi wasioona na Walimu wao Wilaya ya Wanging’ombe. Baadhi ya vitu alivyotoa ni pamoja na T-Shirt (25) na kiasi cha Shilingi Milioni Moja Taslimu kwa ajili ya usafiri na vinginevyo.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Upatikanaji wa Teknolojia fikivu katika Ujenzi wa Uchumi wa Kidijitali ni MKOMBOZI kwa mtu asiyeona na Taifa”.