HALMASHAURI ya Wilaya ya Wanging'ombe imeendelea kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan linalohusu udhibiti wa magonjwa yasiyoambukizwa kupitia mazoezi ya viungo.
Mazoezi hayo yamefanyika Viwanja vya Shule ya Sekondari ya Igwachanya ambapo yamehusisha watumishi wa umma na wanafunzi wa sekondari hiyo yamesaidia kudumisha umoja na ushirikiano baina ya taasisi za serikali zinazoshiriki pia kuboresha afya za watumishi wa umma ambao muda mwingi wamekuwa wakifanya shughuli zao wakiwa katika mazingira ya kukaa mahala pamoja.
Akiongea baada ya hitimisho la mazoezi hayo, Katibu Tawala, Wilaya ya Wanging'ombe, Bi. Veronica Gerald amesema wanatazamia kuanzisha klabu ya michezo ya riadha kwa watumishi wa umma (Jogging Club) ili kuimarisha ukakamavu na kupunguza magonjwa yasioambukizwa.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji, Wanging'ombe, Dkt. Peter Maiga Nyanja amesema watumishi wote watatakiwa kushiriki mazoezi hayo kwa kuzingatia umbali utakaowekwa na wataalamu/wakufunzi wa mazoezi ili kuepusha athari mbalimbali.
Aidha mahudhurio ya watumishi wa umma yameendelea kuongezeka kadiri ya uhamasishaji unaofanywa na Afisa Maendeleo ya Michezo, Utamaduni na Sanaa, Bi. Anitha Kivike kwa uzingatiaji wa agizo la Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.