MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KUWEZESHWA VISHIKWAMBI 18 -WANGING’OMBE
Tarehe iliyowekwa: August 27th, 2025
Na. Nickson Kombe,
KAIMU Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Bw. Onolasco Mwogofi amekabidhi vishikwambi 18 kwa maafisa maendeleo ya jamii kata ikiwa lengo ni kuongeza ufanisi wa kazi na utoaji huduma kwa wananchi wilayani Wanging’ombe.
Bw. Mwogofi ameyasema hayo leo Agosti 27, 2025 wakati akizungumza katika hafla fupi ya Idara hiyo iliyofanyika ofisi za Halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe kwa ajili ya kuhamasisha maafisa hao kuendelea kutoa huduma iliyo na viwango vya juu kwa wananchi kwa ufanisi unaotazamiwa na taasisi.
Hata hivyo maafisa maendeleo ya jamii wameelekezwa kuacha kukaa maeneo ya mjini pekee na badala yake wajitahidi kufikia vikundi mbalimbali vinavyofanya shughuli za maendeleo ikiwa lengo ni kuwashauri na kuwawezesha kuendeleza shughuli hizo na kuleta maendeleo kwenye jamii.
Aidha Idara ya maendeleo ya jamii inatazamia kuwafikia na kutoa huduma kwa zaidi ya Asilimia 75 ya vikundi vyote vilivyoomba mikopo kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo.