MAADHIMISHO YA SIKU YA AFYA NA LISHE KWA VIJANA BALEHE - WANGING'OMBE
Tarehe iliyowekwa: October 28th, 2023
Na. Nickson Kombe,
Kuelekea kilele cha maadhimisho siku ya Afya na Lishe kwa Vijana Balehe, kitaifa yanayotarajiwa kufanyika Mkuranga, Mkoani Pwani. Wilaya ya Wanging'ombe imeadhimisha katika Kata ya Igwachanya, tarafa ya Mdandu ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni "Lishe Bora kwa Vijana balehe, Chachu ya Mafanikio Yao".
Akihotubia katika hafla fupi, Afisa Tarafa ya Mdandu, Bw. Emmanuel Kingu amewaasa wazazi kuzingatia lishe bora yenye virutubisho vyote ili kuboresha afya ya mwili na akili kwa watoto na familia kwa ujumla. Amenukuliwa akisema "Wilaya yetu imekua na matokeo mabaya baada ya tafiti za lishe, ijapokuwa tunalima na tunauza mazao mengi sana..., hivyo elimu ya lishe katika ngazi ya kaya iboreshwe zaidi ili kuhakikisha tunabadilisha utamaduni wa chakula kwa kuzingatia lishe bora..." ameyasema haya akiwa amealikwa kuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo.
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya, Bw. David Hunja amesema ukosefu wa lishe bora kwa watoto na vijana umekuwa na athari ambazo hupelekea udhaifu wa mwili na akili, kupungua kwa kinga na kukaribisha magonjwa ya moyo, shinikizo la juu la damu, saratani, kisukari, magonjwa ya figo n.k. Hivyo vijana wanapaswa kuzingatia lishe bora ili kukomboa taifa la baadae.
Utamaduni wa kuzingatia lishe bora unaendelea kuenezwa kwa vitendo, namna bora ya kufanya shughuli za kilimo bila kutumia viwatilifu vya kiwandani, ufugaji wa kuku na wanyama wengineo, unywaji wa maji mengi, kupunguza na kuacha matumizi ya vileo, dawa za kulevya, kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta, sukari na chumvi kwa wingi n.k. Jitahada zote hizo zimeendelea kufanywa kwa kuzingatia jamii inapata elimu ya lishe bora amesema hayo Afisa Lishe Wilaya, Bi. Zenobia Aloyce.
Aidha wazazi waaswa kuacha unyanyasaji kwa watoto, kutelekeza familia na kutozingatia ustawi wa familia, kukwepa majukumu yao ya msingi ambapo imeelezwa kuwa ndizo sababu zinazopelekea lishe duni kwenye familia.
Kwa upande wa Wananchi waliohudhuria hafla hiyo wameshukuru kwa kupata uelewa ya kuwa "Ni kheri kunywa lita moja ya maziwa kuliko vilevi..." ameyasema hayo Mwenyekiti wa Igwachanya.