MKUU wa mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka amemuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe Bi .Amina Kiwanuka kuhamisha fedha milioni mia 3 zilizopelekwa katika zahanati ya Palangawanu kupelekwa katika kituo cha afya cha Wanging’ombe mara moja kwaajili ya ukarabati wa kituo hicho.
Sendeka alifikia uamuzi huo mara baada ya kubaini mchezo mchafu uliofanywa na baadhi ya viongozi na kusababisha mkanganyiko wa fedha hizo ambazo zilikuwa kiasi cha shilingi milioni mia 4 na kuahidi kuwachukulia hatua bila kujali ni kina nani kwa kuwa bila kufanya hivyo yeye atafukuzwa kazi.
“Mpango wa ukarabati wa zahanati hizo siyo mradi uliyoibuliwa na wananchi wala madiwani bali ni mradi wa serikali kuu hivyo kitendo cha kubadilisha fedha na kuzileta katika zahanati ya Palangawanu ni makosa makubwa na kitendo hiki siwezi kukifumbia macho,” alisema.
Alisema serikali kupitia Ofisi ya rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iliamua kukarabati vituo vya afya mia moja nchi nzima ili kuboresha huduma ya afya hasa kwa upande wa upasuaji ndipo walipotenga fedha kwaajili ya kazi hiyo na zahanati ya Wanging’ombe mkoani Njombe ilifanikiwa kuingia katika mchakato huo.
Aliongeza kuwa baada ya kukamilika kwa mchakato huo fedha za awamu ya kwanza kiasi cha shilingi milioni mia 4 zilitolewa kwaajili ya kituo cha Wanging’ombe lakini kuna baadhi ya viongozi walienda kuwalaghai maafisa wa TAMISEMI na kuwataka kuzituma fedha hizo katika kituo cha afya cha Palangawanu.
“Kituo hiki hakina sifa ya kupata fedha hizo kwa kuwa ni zahanati ila kwasababu ya ushawishi waliokuwa nao watu hao walifanikiwa kuwalaghai maafisa wa TAMISEMI na kuzipeleka fedha hizo kusikotakiwa na ahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria watu hao pindi nitakapowabaini,” alisema.
Aidha alibainisha kuwa fedha hizo mara baada ya kufika katika zahanati hiyo zilianza kazi na baada ya wiki moja mchezo huo ulibainika na zoezi la ujenzi wa zahanati hiyo ulisitishwa mpaka suala hilo litakapo zungumzwa na kuwekwa sawa.
Mpaka jana mkuu wa mkoa ana muamuru mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe kurudisha fedha hizo kwenye akaunti ya kituo cha afya cha Wanging’ombe tayari kiasi cha shilingi milioni mia moja zilishatolewa na kiasi cha shilingi milioni 32 zimeshatumika na milioni 28 ni madeni ambayo wanatakiwa kulipa watu wanaowadai.
Kufuatia hali hiyo Sendeka aliwataka kuchukua kiasi hicho cha shilingi milioni mia moja na kuhakikisha wanakarabati zahanati ya Palangawanu mpaka ikamilike kwa kushirikiana na wananchina kiasi cha shilingi milioni mia 3 zilizobaki kuzipeleka katika akaunti ya kituo cha afya cha Wanging’ombe.
Wakati huo huo aliwataka wanasiasa wanaoendesha siasa za maji taka na kuwashauri wananchi kuacha kuchangia miradi ya maendeleo kuacha siasa hizo mara moja na kuahidi kuwashughulikia.
“Wanasiasa wanaoendesha siasa za maji taka nitashuka na nyie vinginevyo mjirekebishe haraka,” alisema
Kwa upande wake diwani wa kata ya Wanging’ombe Geofrey Nyagawa alisema januari mosi 2018 ni siku ambayo wananchi wa Wanging’ombe walichukia mno mara baada ya kusikia fedh hizo zimepelekwa Palangawanu lakini Februari 8 ni siku ambayo wamefurahi kupata haki yao ya msingi mara baada ya mkuu wa mkoa kumuamuru mkurugenzi kufanya hivyo mara moja kabla ya februari 10 .
Naye katibu mkuu kiongozi mstaafu Philemoni Luhanjo alimpongeza mkuu wa mkoa wa Njombe kwa kusimamia mkoa vizuri na kutoa maamuzi ya haki kwa wananchi wake.
“Siyo sahihi viongozi kuwahujumu wananchi wao kwa kuwa wao ndiyo wasimamizi wa haki za wanachi wao wanapokuwa mstari wa mbele kuipoteza haki wanapoteza imani kwa watu wanaowaongoza,” alisema.
MWISHO
Copyright ©2021 Wanging'ombedc . All rights reserved.