KAMATI YA FEDHA, UONGOZI NA MIPANGO (KFUM) YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI MRADI WA UJENZI MIUNDOMBINU YA MADARASA (KIDATO CHA 5 NA 6) SHULE YA SEKONDARI MAKOGA - WANGING'OMBE
Tarehe iliyowekwa: October 16th, 2023
Na Nickson Kombe,
16 Oktoba 2023.
Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango (KFUM), Mhe. Onesmo Lyandala akiambatana na Wajumbe wa Kamati hiyo ameridhishwa na utekelezaji mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Madarasa, matundu ya vyoo na mabweni ya Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Sekondari, Makoga.
Akitoa mrejesho wa Taarifa ya Ujenzi wa Miundombinu hiyo, Mhe. Onesmo Lyandala ameridhika namna ambavyo utaratibu wa Force Account umeharakisha utekelezwaji wa miradi hii ya maendeleo ulipoanza kutumika tarehe 06 Agosti 2023.
Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Wanging'ombe, Bi. Maryam Muhaji akitolea ufafanuzi mbinu mbadala zilizotumika katika utekelezwaji wa mradi huu ni pamoja na manunuzi ya vifaa vya ujenzi vyote, ufuatiliaji wa karibu na mara kwa mara, usimamizi mzuri wa fedha ndivyo vimeleta matokeo chanya katika utekelezaji wa mradi wa ujenzi ambao umeigharimu Serikali Shilingi Milioni 744 ikiwa ni Ujenzi wa Madarasa - 8, mabweni - 3, matundu ya vyoo - 12.
Hata hivyo Mkuu wa Shule, Mwl. Lize Mulungu ametoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Naibu Waziri (Ofisi ya Rais - TAMISEMI), Mbunge wa Jimbo la Wanging'ombe, Mhe. Dkt. Festo Dugange na Diwani Kata ya Makoga, Mhe. Jaros Lunyungu kwa mchango wao wa kusukuma gurudumu la maendeleo ya sekta ya Elimu.
Aidha Wajumbe wa Kamati hiyo wamesisitiza muendelezo wa uharaka wa utekelezwaji wa mradi huo ili kutoa fursa kwa ongezeko la wanafunzi wanaomaliza Shule za Sekondari, Kidato cha Nne kujiunga na Kidato cha Tano.