IDARA YA AFYA YAFANYA KIKAO CHA TATHMINI YA MKATABA LISHE NGAZI YAWILAYA,WANGING’OMBE
Tarehe iliyowekwa: November 3rd, 2023
Na Mwandishi Wetu,
Rukia Omary.
Mkuu wa Wilaya Wanging’ombe Mhe. Claudia Kitta amezungumza na watendaji wa Kijiji/kata katika kikao cha Tathmini ya Mkataba wa Lishe ngazi ya Wilaya kupokea ajenda na Kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa viashiria vya mkataba wa lishe ngazi ya jamii katika kata 21 yenye vijiji 108.
Mkuu wa Wilaya Mhe. Claudia Kitta amesema Wilaya ya Wanging’ombe ni miongoni mwa wilaya inayopambana kuhakikisha inatokomeza udumavu na ukosefu wa lishe, amewataka Watendaji wote kutoa elimu kuhusu lishe kwa wananchi itakayowasaidia kupambana dhidi ya udumavu; kuwa na ubunifu wa kimaendeleo utakaoleta utofauti baina ya Kata, na kuhakikisha ulinzi na usalama kwa raia. Hata hivyo ametilia mkazo hasa shuleni wanafunzi wapewe chakula chenye mchanganyiko wa virutubisho ili kuwajenga kiafya na akili shule nyingi sana Wilayani zinalima bustani za mbogamboga ambazo zinaongeza protini mwilini hivyo hata majumbani wazazi wajitahidi kutumia makundi haya ya chakula kuimarisha afya.
Afisa lishe Wilaya ya Wanging’ombe Bi. Zenobia Moshi amefafanua kuwa kuhakikisha utekelezaji wa tathmini ya viashiria vya lishe wilaya kila robo ya Mwaka tunapokea taarifa kutoka kwa watendaji wa kata zote kufanya majadiliano na kutolea uvumbuzi wakati wa utekelezaji ili kubaini kama tatizo hili linatatulika kwa aslimia ngapi na kuchukua hatua zaidi.
Hata hivyo, kwa niaba ya watendaji wengine Mwenyekiti wa watendaji Wilaya ya Wanging’ombe Bw. Festo Mbakilwa amefafanua katika kuhakikisha kuwa elimu hii ya lishe inawafikia wananchi watendaji wote kwa umoja wetu tutahakikisha tunalipa motisha hata kwa wanaume kuhudhuria semina za elimu ya lishe ili iwasaidie kuimarisha familia zao na kulitokomeza zaidi na kuwapa onyo wanaume wanaotumia chakula cha Watoto (maziwa ya mama) kama chakula mbadala na kuwanyima haki Watoto kuacha tabia hii ni ukatili kwa Watoto.