FURSA ZA VIBARUA ZATANGAZWA MRADI WA UJENZI SHULE MAALUMU YA WASICHANA YA MKOA, KIJIJI CHA USALULE, KATA YA ULEMBWE - WANGING'OMBE
Tarehe iliyowekwa: October 16th, 2023
Na. Nickson Kombe,
16 Oktoba 2023.
Ziara ya Ukaguzi wa Miradi na Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango (KFUM) imeshauri ongezeko la vibarua wa ujenzi ikiwa na dhumuni la kufanikisha ukamilishwaji wa mradi huo tarehe 30 Disemba 2023.
Akitoa mrejesho baada ya kusomewa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango (KFUM), Mhe. Onesmo Lyandala amesema wananchi waliopo karibu na mradi huo pamoja na vijana wa Wanging'ombe wenye ujuzi na uwezo wa kufanya shughuli za ujenzi wafike eneo la mradi na kuwasiliana na Mhandisi wa Mradi, Joseph Masasi ili awapangie majukumu mbalimbali ya ujenzi chini ya usimamizi wa mafundi.
Mkurugenzi Mtendaji, Wilaya ya Wanging'ombe, Bi. Maryam Muhaji akisisitiza ongezeko la nguvukazi katika utekelezaji wa mradi huo, amesema changamoto ya upatikanaji wa nishati ya umeme eneo la mradi inatafutiwa ufumbuzi ili kazi zifanyike masaa 24 kwani mradi huo ni mkubwa na una thamani ya Shilingi Bilioni 4.1 ambapo ni ujenzi wa vyumba vya madarasa - 22, mabweni - 9, nyumba za walimu - 5, jengo la utawala - 1, bwalo - 1, jengo la TEHAMA, Maktaba, Maabara - 4 na Matundu ya Vyoo - 16.
Hata hivyo Wajumbe wa Kamati hiyo wamesisitiza wataalamu kushirikiana kufanya kazi ili kufanikisha utekelezwaji wa mradi huo uliochelewa kutokana na zoezi la uvunjaji mikataba na kandarasi mbalimbali hapo awali.
Aidha Mhandisi wa Mradi, Joseph Masasi ameweka kambi eneo la mradi kuhakikisha uhitaji wa mafundi, ushauri wa kitaalamu, usimamizi wa karibu unafanyika kwa wakati na utekelezwaji wa mradi huo ukamilike kwa muda uliopangwa.