ELIMU YA MATUMIZI SAHIHI YA DAWA NA VIFAA TIBA KWA WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI IGWACHANYA
Tarehe iliyowekwa: October 13th, 2023
Na. Rukia Omary,
13 Oktoba 2023
Maafisa wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Nyanda za Juu Kusini wametoa elimu ya matumizi sahihi ya Dawa na Vifaa Tiba kwa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Igwachanya Wilayani Wangingómbe ikiwa ni wajibu wao kutekeleza sera ya Afya.
Elimu hiyo imetolewa na Afisa Uhusiano, Bi. Maria Sanga ameelezea kuhusu wajibu na shughuli zote zinazofanywa na Mamlaka hiyo (TMDA) ikiwemo kujiridhisha na ubora wa dawa (bidhaa), kusajili viwanda vyote vyenye kutengeneza vifaa tiba, ukaguzi wa dawa (bidhaa) zikiwa sokoni na kukusanya taarifa (data) kutoka kwa watumiaji waliopatwa na madhara/athari mbalimbali baada ya matumizi ya dawa. Pia kufanya uchunguzi wa vifaa tiba na dawa kupitia maabara kubwa maalumu zinazotambulika na serikali ili kubainisha usalama wa vifaa hivyo kwa watumiaji.
Kwa upande wa Afisa Mkaguzi wa Dawa, Adam Sarota amesema matumizi mabaya ya dawa hupelekea madhara katika mwili wa binadamu haswa katika figo na maini ambavyo huathirika kwa haraka na kemikali ambazo zisipotumika kwa kiwango sahihi hupelekea sumu. Hata hivyo yapo mambo mgonjwa anatakiwa kuzingatia wakati anatumia dawa hizo, pia anapaswa kuwa na uhakika wa dawa anazotumia kwa kuzingatia muda sahihi wa dozi ya dawa hizo.
Mafunzo hayo yamekuwa na ushirikishwaji haswa kwa Wanafunzi kupewa fursa za kuuliza maswali, kutoa maoni, changamoto na ushauri nini kifanyike ili kuboresha uhusiano baina ya taasisi hiyo, jamii na watoa huduma za madawa ikiwa na lengo la kufichua na kupunguza athari mbalimbali zitokanazo na utumiaji wa dawa zisizo salama kwa afya ya binadamu.
Aidha Maafisa wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) wametumia fursa hiyo kushukuru uongozi wa Shule ya Sekondari Igwachanya na Halmashauri ya Wilaya ya Wangingómbe kwa ushirikiano wao katika kutekeleza sera za afya katika wilaya hiyo. Programu hii ni mahususi na endelevu kwa ajili ya Utoaji Elimu kwa Umma yenye Kauli Mbiu “TMDA – Hulinda Afya ya Jamii”.