MKUU wa Wilaya ya Wanging’ombe, Mhe. Zakaria Mwansasu amewaasa wanafunzi na wazazi kuzingatia elimu bila ya kujali umri wao ikiwa ni kuelekea kilele cha maadhimisho ya juma la Elimu ya Watu Wazima yaliyofanyika kata ya Ilembula Agosti 26, 2025 wilayani Wanging’ombe.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Mwansasu ameeleza namna Serikali ilivyojizatiti kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa wananchi wa rika zote.
Hata hivyo amewataka wazazi kuwasimamia vyema watoto wao wawapo shuleni na nyumbani ili wazingatie elimu na kuepusha tabia za utoro pamoja na matendo yasiyofaa ambayo hupelekea ukatili wa kijinsia.
"Hatuwezi kukubali watoto wetu kufeli, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan analeta fedha nyingi ili wanafunzi wasome na wafaulu, natamani wazazi tuwalee watoto wetu kwa ubora kama sisi tulivyolelewa" alisema Mhe. Mwansasu.
Katika kuhakikisha elimu inaimarika, mwaka 2021 Serikali ilianzisha miradi mbalimbali ikiwemo SEQUIP na MEMKWA ambayo imewasaidia wasichana na wavulana walioacha shule kutokana na changamoto mbalimbali waweze kurejea kwenye masomo.
Adam Wella ni mmoja wa wanafunzi wa Darasa la 6 alienufaika na miradi hiyo kwa kumuwezesha kurudi shule baada ya kupata changamoto zilizopelekea kukatisha masomo yake."Nilianza elimu ya watu wazima mwaka 2020, nilihamasika kujiunga na elimu hii baada ya kumsikia Mhe. Rais akitutaka turudi shuleni" alisema Adam" Nilikata tamaa kabisa baada ya kukumbwa na changamoto, nilipata nafasi kuanza masomo katika shule ya msingi Igdeledza, Ilembula, nawaomba vijana wenzangu wasikate tamaa na warudi shuleni kutimiza malengo yao" aliongeza.
Kwa sasa, Halmashauri kupitia Idara ya Elimu Msingi imeendelea kusimamia na kuwapa kipaumbele wanafunzi wa namna hiyo ili kutoa hamasa kwa jamii na kuhakikisha wanatekeleza, kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha elimu.
Aidha Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima kwa mwaka 2025 yameongozwa na kauli mbiu isemayo "Kukuza kisomo katika zama za Kidijitali kwa maendeleo endelevu ya taifa letu"