DC MWANSASU: WEZESHENI SHULE UFUGAJI WA KUKU ILI KUBORESHA HUDUMA ZA LISHE BORA – WANGING’OMBE
Tarehe iliyowekwa: July 31st, 2025
Na. Nickson Kombe,
MKUU wa wilaya ya Wanging’ombe, Mhe. Zakaria Mwansasu ameelekeza kamati za lishe katika halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe kufanya ununuzi wa vifaranga vya kuku 4,500 katika shule tisa (9) ili kuboresha huduma za lishe pia ni utekelezaji wa kampeni ya lishe mkoani Njombe.
Akiongea na wajumbe hao katika kikao cha Robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/25, Mhe. Mwansasu amesema iwapo shule za majaribio hayo zimeshakamilisha maandalizi ya mabanda ya kisasa ya ufugaji wa kuku hao, basi Halmashauri inatakiwa kutenga sehemu ya bajeti yake na kufanya ununuzi wa vifaranga vya kuku 4,500 katika shule tisa (9) ili kuboresha huduma za lishe bora ambapo kila shule itapokea vifaranga 500 wilayani humo.
Hali kadhalika utekelezaji wa zoezi hilo utaenda kuboresha huduma za lishe bora, “kwanza kwa kuwapatia wanafunzi mbinu za ufugaji kuku, kuongeza umuhimu wa kupata mlo kamili na kupata kitoweo kwa urahisi zaidi katika mlo wa wanafunzi hao huko mashuleni, kitu ambacho kitaenda kuleta matokeo mazuri zaidi…..” ameyasema hayo Mhe. Mwansasu.
Aidha wajumbe wa kikao hiko cha lishe katika Halmashauri wamelipokea hilo na kuahidi utekelezaji mapema iwezekanavyo katika bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 ili kufikia lengo la kampeni ya lishe katika mkoa wa njombe yenye kauli mbiu: Lishe ya Mwanao, Mafanikio yake – “Kujaza tumbo si Lishe, Jali unachomlisha”.