DARASA DIGITALI KUPUNGUZA MAKALI YA UPUNGUFU WA WALIMU WA SAYANSI SEKONDARI – WANGING’OMBE
Tarehe iliyowekwa: July 31st, 2025
Na. Nickson Kombe,
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Mawasiliano la Tanzania (TTCL) wamebuni mfumo wa TEHAMA ambao unatoa fursa kwa Mwalimu mmoja kufundisha madarasa zaidi ya moja katika maeneo/shule tofauti ikiwa lengo ni kuhakikisha wanafunzi wote wanapata fursa ya kujifunza masomo husika kwa wakati.
Akiongea na waandishi wa Habari, Mtaalamu wa Mifumo ya TEHAMA, Bw. Fortunatus Salmin amesema zimefanyika tafiti za kutosha na kufanikisha ubunifu huo ambao utaenda kufanya mapinduzi katika sekta ya elimu na kupunguza makali ya upungufu wa walimu wa sayansi katika sekondari ambapo ufanisi na ufaulu wa wanafunzi utaongezeka zaidi.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe, Dkt. Peter Maiga Nyanja amesema mifumo ya TEHAMA itaenda kusambazwa zaidi mashuleni wilayani humo na sehemu ya bajeti katika mapato ya halmashauri yataelekezwa katika miradi ya TEHAMA ili kuboresha sekta ya elimu na kuongeza ufanisi pia kupambana na changamoto ya upungufu wa walimu wa sayansi.
Aidha mfumo huo ambao umefanyiwa mazoezi mkoa wa Njombe katika shule za sekondari za Igwachanya – Wanging’ombe, Mabatini – Njombe Mjini na Makambako, ambapo Mwalimu wa Kemia amefundisha madarasa matatu kutokea Mabatini – Njombe Mijini na amefanikiwa kwa asilimia kubwa kitu ambacho kimepelekea halmashauri za mkoani Njombe kujipanga kuendelea kuwezesha shule za sekondari ili kufikia lengo la uhitaji wa vifaa vya TEHAMA.