DAKTARI NYANJA AZINDUA ZOEZI LA UGAWAJI VITENDEAKAZI, SEKTA YA MIFUGO.
Tarehe iliyowekwa: September 21st, 2025
Na. Nickson Kombe,
MKURUGENZI Mtendaji, Halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe, Dkt. Peter Maiga Nyanja amezindua zoezi la ugawaji wa vitendeakazi kwa maafisa mifugo na kusisitiza kwamba vifaa hivyo vitumike katika kuboresha mchakato wa utoaji huduma kwa jamii za wafugaji ili kuinua afya ya mifugo yao na si kwa matumizi mengineyo.
Akizindua zoezi hilo leo Jumamosi Septemba 20, 2025 katika ukumbi wa Halmashauri, Dkt. Nyanja amesema Serikali haitarajii kuona vitendea kazi hivi vinazagaa mtaani na pengine kumilikishwa kwa wasiohusika.
Dkt. Nyanja akaendelea kusema lengo la ugawaji wa vitendeakazi hivyo kwa maafisa mifugo wote wilayani ni katika kuboresha na kutoa huduma kwa jamii za wafugaji, hivyo wameaswa kuwa mfano katika jamii zinazowazunguka.
Mkurugenzi, Dkt. Nyanja akaendela kusema Serikali awamu ya sita inayoongozwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa vitendo kuwekeza katika eneo la Mifugo ili kuwawezesha vijana kupata ajira na kuzalisha ajira na kukuza uchumi kupitia shughuli mbalimbali.
Kwa hivyo vishikwambi 32, boksi maalumu la kubebea na kusafirisha chanjo (coolbox) 10, buti maalumu za kazi 10, vifaa vya kuvalishia hereni za ng'ombe 2, hereni za ng'ombe 77,000, automatic syringe 10, chanjo za ng'ombe 77,000, chanjo za kuku 270,000, pesa taslimu kwa ajili ya chanjo na utambuzi 20,900,000 na vifaa vinginevyo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kukabidhiwa maafisa mifugo.
Aidha Mwakilishi wa Maafisa Mifugo, Dkt. Mfikwa ametumia fursa hiyo kuwakumbusha maafisa hao jinsi ya kuwajibika na kuwa karibu ki vitendo ili jamii za wafugaji ziige mazuri.