BARAZA LA MADIWANI WANGING’OMBE LAPINGA MUENDELEZO WA MATUMIZI YA DAMPO LA ITENGELO KAMA ENEO RASMI LA KUTUPA TAKA ZA MJI WA MAKAMBAKO
Tarehe iliyowekwa: October 31st, 2023
Na Mwandishi Wetu,
Nickson Kombe,
Baraza la Madiwani, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe wamepinga vikali kitendo cha matumizi sehemu ya eneo lililopo Kijiji cha Itengelo, Kata ya Saja, Wanging’ombe kama sehemu ya kutupa taka za mji wa Makambako.
Akiongea katika baraza la madiwani la mwezi Oktoba, Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Onesmo Lyandala amesema wameazimia kwa pamoja kupinga matumizi ya eneo hilo kama eneo rasmi la kutupa taka za mji wa Makambako, kutokana na uchunguzi uliofanywa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na kubaini ya kuwa kuna muingiliano mkubwa wa taka hizo na mifereji ya maji iliyopo karibu na sehemu hiyo.
Ardhi hiyo iliyopo Kijiji cha Itengelo, Kata ya Saja inayokadiriwa kuwa ekari 25, eneo hilo linamilikiwa na mtu binafsi. Kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa matumizi ya ardhi hiyo, ambapo Halmashauri ya Mji wa Makambako wameendelea kutumia eneo hilo kama dampo rasmi la kutupa taka za mji huo muda mrefu. Kipindi cha mgawanyo wa ardhi za Halmashauri 2010, eneo hilo lilikuwa ndani ya umiliki wa Halmashauri ya Njombe, baadae Mwaka 2012 likamilikishwa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe. Idhini ya muendelezo wa matumizi ya eneo hilo iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mnamo wa Julai 2016, na baadae Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kutoa katazo la kimazingira mnamo wa Februari 2019 “Environmental Protection Order” kuzingatia sheria ya mazingira 2004 ambayo “imeweka bayana kila Halmashauri husika kutenga maeneo ya taka ndani ya mipaka yao…na sio vinginevyo” ili kuepusha migogoro na kuendelea kutunza mazingira kwa kufuata taratibu zote za uhifadhi wa mazingira bila athari.
Hata hivyo dampo hilo la Itengelo kijografia lipo karibu na chanzo cha maji kinachotiririsha maji kuelekea kitongoji cha Makonda. Kipindi cha mvua mifereji ya maji hupelekea muingiliano wa taka hizo na kuleta athari kwa watumiaji wa maji hayo.
Aidha Baraza la madiwani wamepinga hilo ili kuepusha athari za kimazingira zinazotokana na muendelezo wa kutupa taka katika dampo hilo.