Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe ametoa wito kwa wananchi wa kata ya Wangama kuweza kushiriki kuchangia nguvu katika ujenzi wa Kituo cha Afya kinachojengwa katika kata hiyo,Mhe Mkuu wa Wilaya ameyasema hayo leo Tarehe 12/3/2022 akiwa katika kata ya Wangama akizindua ujenzi wa Kituo cha afya “.Ninawaomba sana Wananchi muweze kujitolea kwa kiasi kikubwa nguvu zenu ili ujenzi wa kituo hiki cha afya unaojengwa kwa mapato ya ndani uweze kukamilika kwa haraka ili kuunga jitihada za Halmashauri “Alisema Mhe Mkuu wa Wilaya Lautery John Kanoni.
Hafla ya uzinduzi ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bi Maryam Muhaji , Mhe Diwani wa Kata Mhe Mwalongo,Mganga Mkuu Dr Frank Chiduo,Afisa Mipango Ndg Niceforus Mgaya na Mtendaji wa Kata hiyo Upendo Fute.
Mkurugenzi Mtendaji Bi Maryam Muhaji amesema Halmashauri imeamua kujenga Kituo cha Afya Wangama kwa kutumia Mapato yake ya Ndani ikiwa ni kutekeleza agizo la Serikali la Kujenga Kituo cha Afya kulingana na Makusanyo yake ya Ndani.”Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe katika bajeti yake ya mwaka 2021/2022 imetenga Jumla ya Kiasi cha Tsh 250,000,000/= kwa ajili ya kuanza kujenga Kituo hicho ambapo mpaka sasa Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani imeshapeleka Jumla ya Tsh 100,000,000/= kwa ajili ya Ujenzi huo pia kiasi cha Tsh 250.000.000/= kimetengwa katika Bajeti ya Mwaka 2022/2023 ili kukamilisha kiasi cha Tsh 500,000,000/= kinachohitajika kukamilisha ujenzi huo”. Alisema Mkurugenzi Mtendaji.
Aidha akielezea utaratibu wa Ujenzi huo Mganga Mkuu wa Wilaya Daktari Frank Chiduo amesema majengo yatakayo jengwa ni majengo saba yenye thamani ya Tsh 500,000,000/= ikiwa ni Jengo la wagonjwa wa nje,Jengo la Mama na Mtoto, Jengo la Upasuaji,Jengo la Maabara,Jengo la kuhifadhia Maiti, Jengo la Kufulia na Nyumba ya Mtumishi kwa sasa utekelezaji unaanza na Ujenzi wa Jengo la Wagojwa wa nje yaani OPD.
Nae Mheshimiwa Diwani wa kata ya Wangama Mhe Mwalongo alitoa shukrani kwa Serikali kwa kuamua kujenga Kituo cha afya katika kata yake amesema kituo hicho kitakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wake, alimhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa Wananchi watashiriki kikamilifu kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wananchi kutoa mchango wao katika ujenzi huo.
Copyright ©2021 Wanging'ombedc . All rights reserved.