Utekelezaji Operesheni Anwani za Makazi wafikia asilimia 67
Na. Fred Kibano, OR - TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mheshimiwa Innocent Bashungwa amesema kazi ya utekelezaji wa operesheni ya anwani za makazi kwenye mikoa yote Tanzania Bara imefikia asilimia 67 ya utekelezaji wake.
Waziri Bashungwa ameyasema hayo wakati wa kikao kazi kati ya Wakuu wa Mikoa, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia kuhusu uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa operesheni ya anwani za makazi nchini Jijini Dodoma hii leo.
“tumefikia asilimia 67 lakini bado tuna kazi kubwa ya kufanya, sina shaka na Wakuu wa Mikoa, naamini hili la operesheni ya Anwani za Makazi mtafanya vizuri” ,alisema Waziri Bashungwa.
Aidha, Waziri Bashungwa amesema kwa sasa kazi iliyobakia ni kuongeza hamasa kwenye kazi hiyo na kutoa elimu kwa wananchi ili kazi hiyo iendelee vizuri na kufikia malengo yanayotarajiwa na Serikali.
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nnape Nnauye amesema zoezi la utekelezaji wa operesheni ya anwani za makazi limekwenda vizuri na linatarajiwa kukamilika kabla ya muda uliopangwa ambao ni tarehe 22 Mei, 2022 ikiwa ni pamoja na kukamilisha Mfumo wenyewe wa anwani za makazi ambao upo chini ya wizara yake.
Waziri Nape Nnauye amesema kwa hivi sasa Serikali inaendelea kutambua maoni yaliyotolewa, kutoa elimu kwa wananchi, kuandaa taarifa, kutengeneza taarifa hizo na kuziingiza kwenye mfumo ikiwa ni pamoja kuuweka mfumo wenyewe ili ufanye kazi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe amesema lengo la kikao kazi ni kujadili namna ambavyo Wakuu wa Mikoa wanaendelea kutekeleza operesheni ya anwani za makazi Tanzania Bara lakini pia zoezi hili linaendelea na Zanzibar kazi ambayo inakwenda sambamba na Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mwezi Agosti, 2022.
Mwenyekiti wa Wakuu wa Mikoa ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela amesema zoezi la anwani za makazi linaendelea vizuri kama ambavyo wizara iliwapa maelekezo kwani fedha za kazi hiyo zilipokelewa ijapokuwa kuna maeneo machache ambayo yalikuwa na tatizo la kimtandao wakati wa kutumia fedha za kazi hiyo.
Amesema baadhi ya changamoto zilijitokeza ni uwingi wa watu kwa baadhi ya mikoa pamoja na maeneo makubwa ya makazi lakini wanashukuru wizara zilituma timu za wataalam katika kusaidia utekelezaji wa kazi hiyo.
Zoezi la anwani za makazi linafanywa na wizara mbili kwa pamoja ambazo ni Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ambalo linatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 22 Mei mwaka huu kama ilivyoagizwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wakati akilizindua mnamo Februari, 8 mwaka huu.
|
Copyright ©2021 Wanging'ombedc . All rights reserved.