Na. Nickson Kombe,
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe, Dkt. Peter Maiga Nyanja amewapongeza timu yote ya mapato kwa kufikia asilimia 71 ya lengo la ukusanyaji mapato mwaka wa fedha 2025/26 katika kikao kazi kilichofanyika Ukumbi wa Halmashauri.
Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 06 Februari 2026, wakati akizungumza na timu ya wakusanya mapato wa Halmashauri, Dkt. Nyanja amesema anatarajia ifikapo machi 2026, timu hiyo itakua imevuka malengo hivyo waendelee kufanya kazi kwa weledi na ubunifu zaidi ili kudhibiti mianya mbalimbali ya uchepushaji wa mapato ya Halmashauri.
“Pamoja na changamoto zilizopo, natumia fursa hii kuwapongeza kwa ukusanyaji mzuri wa mapato, nimejulishwa ya kuwa mwaka huu mnataka kuvuka lengo na kwa takwimu za wiki iliyopita mmefika asilimia 71 hivyo sina shaka naamini kufikia Machi 2026 mtafuka lengo, hii inaonesha ni namna gani mnafanya kazi kwa kujituma na kwa ushirikiano. Pongezi kwenu,” alisema Dkt. Nyanja.
Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe imepangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 5.4 mapato halisi kwa mwaka wa fedha 2025/2026. hadi kufikia mwisho wa mwezi Mei 2026. Mpaka kufikia mwisho wa mwezi Januari 2026, Halmashauri imekusanya Shilingi Bilioni 3.8 sawa na Asilimia 71 ya lengo, ikiwa ni ongezeko la asilimia 2 ukifananisha na mwaka wa fedha uliopita 2024/25.
Hivyo timu ya wakusanya mapato wa Halmashauri ikiwakilishwa na Mwenyekiti wao, Bw. Frank Kassano ametumia fursa hiyo kutoa neno la shukrani kwa uongozi dhibiti wa Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Peter Maiga Nyanja kwa namna ambavyo amekuwa akiwajali katika maslahi yao, haki na kuwawezesha kufanya kazi katika mazingira rafiki zaidi. Hivyo timu hiyo imemzawadia Mkurugenzi Mtendaji, Dkt. Nyanja zawadi kede kede.
Aidha Mafanikio haya yanaiweka Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe katika ramani ya Halmashauri zinazotekeleza vyema maelekezo ya Serikali ya kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuongeza uwezo wa kuwahudumia wananchi na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati.









Copyright ©2021 Wanging'ombedc . All rights reserved.