SERIKALI IMEWAWEZESHA MAAFISA UGANI MIFUGO USAFIRI WA PIKIPIKI 6 ILI KUWAFIKIA WAFUGAJI WANGING'OMBE.
Tarehe iliyowekwa: February 16th, 2024
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeendelea kuwawezesha Maafisa Ugani Mifugo usafiri wa pikipiki 6 (Cc 125) ili waweze kuwafikia wafugaji mbalimbali katika Wilaya ya Wanging'ombe na kuwasaidia wafugaji kufanya shughuli za ufugaji kwa ubora na utaalamu wenye manufaa kwa taifa na kukidhi mahitaji ya soko.
Akiongea kwenye hafla fupi ya Makabidhiano ya Pikipiki hizo, Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe, Mhe. Claudia Kitta amesema lengo kuu la uwezeshwaji vyombo hivyo vya usafiri ukazingatiwe na Maafisa Ugani Mifugo ili kuleta tija na manufaa yaliyokusudiwa kwa jamii za wafugaji wa wilaya ya Wanging'ombe.
Akifafanua mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosimamiwa na Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkuu wa Wilaya ya Wanging'ombe amesema katika kipindi cha miaka minne (2021 - 2024) Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe imepokea jumla ya pikipiki 45 kutokea Wizara za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi ili kuwawezesha watumishi wa Idara husika kutekeleza majukumu yao ya msingi na kuleta tija na maendeleo ya shughuli za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi.
Hata hivyo Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Ufugaji na Uvuvi imeendelea kusimamia lengo kuu la kutatua changamoto ya upungufu wa vyombo vya usafiri kwa Maafisa Ugani Kilimo (Ushirika), Ufugaji na Uvuvi ili kuongeza tija na kuwasaidia ushauri makundi ya wakulima, wafugaji na wavuvi kufanya shughuli zao kwa utaalamu utakaokuwa bora na manufaa zaidi kwa taifa na soko la bidhaa zao.
Kwa niaba ya Maafisa Ugani, Afisa Ugani Kilimo, Wanging'ombe, Bw. Henry Vahaye ameishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa uboreshaji katika shughuli za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi ambapo kwa miaka ya karibuni kumekuwa na mabadiliko ya kiwango cha juu cha Uzalishaji wa Vyakula, Mifugo na Uvuaji Samaki. Pia Elimu ya kufanya shughuli husika itasambaa zaidi na kusaidia kuleta tija na maendeleo katika Wilaya ya Wanging'ombe