Dodoma.Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuanzia Juni Mosi, itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuuza, kuingiza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote.
“Aidha, ifikapo Mei 31, mwaka huu itakuwa mwisho wa kutumia mifuko ya plastiki kubebea bidhaa mbalimbali. Kuanzia sasa tunatoa fursa ya viwanda kubadili teknolojia yao, wauzaji kuondoa mizigo yao au kumaliza kuuza yote na kadhalika,” alisema Majaliwa jana wakati akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2019/2020 jana jioni.
Alisema, “Ofisi ya Waziri wa Nchi Makamu wa Rais itajiandaa kutumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira ili kulifanya katazo hili kuwa na nguvu ya kisheria. Tunachukua hatua hii kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na miundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki.”
Alisema katika kuchukua hatua hizo kuna bidhaa lazima zifungashiwe kwa mifuko ya plastiki, “vifungashio kwa bidhaa hizo havitapigwa marufuku kwa sasa. Katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, yatatolewa maelezo ya kina kuhusu katazo hili hasa katika maeneo ya uzalishaji wa viwanda, sekta ya afya na kilimo.”
Copyright ©2021 Wanging'ombedc . All rights reserved.