DED WANGING'OMBE AELEZA UTAYARI WA KUPOKEA WANAFUNZI TAREHE 15 JANUARI 2024 SHULE YA SEKONDARI YA WASICHANA MKOA WA NJOMBE - USALULE
Tarehe iliyowekwa: January 8th, 2024
Na. Mwandishi Wetu,
Nickson Kombe.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Wangong'ombe, Dkt. Peter Maiga Nyanja aeleza namna ambavyo wamejipanga kupokea wanafunzi tarehe 15 Januari 2024 Shule ya Sekondari ya Wasichana Mkoa wa Njombe iliyopo Kata ya Ulembwe, Kijiji cha Usalule.
Dkt. Nyanja ameyasema hayo alipokuwa kwenye ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, ambapo amekutana na viongozi mbalimbali wa taasisi za umma akiwemo Meneja wa Mkoa TANESCO Njombe, Meneja wa Mkoa TARURA Njombe na Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Njombe ili kuimarisha ushirikiano na kufanikisha mradi huo.
Akitolea ufafanuzi wa tathmini ya maendeleo ya mradi huo, Dkt. Nyanja amesema miundombinu ya kupokea wanafunzi imekamilishwa kwa asilimia 85 na timu za mafundi zinapambana usiku na mchana kuhakikisha mpaka kufikia tarehe 15 Januari 2024 miundombinu hiyo itakuwa tayari kwa asilimia 100.
Aidha kwa upande wa TANESCO na TARURA wameendelea kutoa ushirikiano wa kufikisha huduma ya umeme na miundombinu ya barabara kuzunguka eneo la mradi ili shughuli nyinginezo zifanikishwe kwa wakati.