DC WANGING’OMBE KUSULUHISHA MGOGORO MPANGO WA UJENZI SHULE YA SEKONDARI KATA, IGIMA
Tarehe iliyowekwa: September 26th, 2023
Na. Mwandishi Wetu,
Nickson Kombe - Wanging'ombe.
Mkuu wa Wilaya Wanging’ombe, Mheshimiwa Claudia Kitta kusuluhisha mgogoro mpango wa ujenzi shule ya Sekondari Kata ya Igima ambapo Kamati ya Maendeleo ya Kata (KAMAKA) baada ya kushindwa kukubaliana ni Kijiji kipi kati ya Lusisi na Nyumbanitu Shule hiyo inatakiwa kujengwa.
Akihutubia Wananchi wa Kata ya Igima, Mh. Claudia Kitta amesema kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaojiunga Sekondari kata ya Igima na kupelekea Shule ya Sekondari iliyopo Kijiji mama cha Igima kuwepo na wanafunzi wengi kuzidi wastani wa Wizara ya Elimu, Serikali kushirikiana na wananchi wa kata ya Igima imeamua kufanya ujenzi wa Shule nyingine ya Sekondari ili kupunguza changamoto za umbali kwa wanafunzi kuelekea mashuleni.
Hata hivyo Mhe. Claudia Kitta ameeleza kuwa kupitia Mwaka huu wa fedha Serikali ina mpango wa kuongeza Shule ya Sekondari Kata ya Igima hivyo ikishirikiana na Wananchi na Kamati ya Maendeleo ya Kata (KAMAKA) wachague eneo linalokidhi vigezo na mpango huo wa Ujenzi wa Sekondari utekelezwe. Ambapo Mwenyekiti wa KAMAKA, Diwani Kata ya Igima, Paulina Samata ameelezea hali ya wajumbe wa Kamati hiyo kushindwa kukubaliana kuhusu Kijiji kipi Sekondari hiyo ijengwe na kuamua kuomba msaada kutoka kwa Wataalamu wa Halmashauri, Wanging’ombe.
Katibu Tawala Wilaya, Veronica Sanga amesema mgogoro huu ni wa kimaendeleo hivyo basi utayari wa wananchi wote kutoka vijiji vya Lusisi na Nyumbanitu ni chachu ya maendeleo ya Kata. Ingawa wanatakiwa kufikia makubaliano kwa sababu bajeti ya mpango wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kata ni kwa ajili ya Shule Moja tu. Hivyo basi kama wataalamu wa Halmashauri walipita kufanya ukaguzi vijiji vyote na kushauri ni Kijiji kipi kinakidhi vigezo vya Ujenzi huo na wakatoa maoni ya kuwa Kijiji cha Nyumbanitu kinastahili kujengwa Shule ya Sekondari Kata, Igima.
Aidha Katibu Tawala Wilaya ametumia fursa hiyo kutoa utaratibu wa upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa.